Ziara ya Katibu Mkuu wa UVCCM, Ndugu Jokate Mwegelo, Chuo cha UVCCM Ihemi
Utangulizi
Mnamo tarehe 21 Juni, nilijaliwa kuwa miongoni mwa watu walioshuhudia ziara ya Katibu Mkuu wa UVCCM, Ndugu Jokate Mwegelo, katika Chuo cha Mafunzo cha UVCCM kilichopo Iheme. Ziara hiyo ililenga kukagua kazi na miradi mbalimbali ya chuo hicho pamoja na maandalizi ya kambi ya makada wa CCM itakayofanyika hivi karibuni.
Chuo hicho cha Ihemi kina historia adhimu katika kulea vijana wa Kitanzania kupitia mafunzo ya mgambo na vilevile katika harakati za ukombozi wa nchi za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.
Historia
Baada ya Azimio la Arusha kutangazwa, ilipopita miaka ya 1970, mkoa wa Iringa kupitia chama cha TANU ulianzisha kambi la Vijana eneo la Igumbiro kwa ajili ya kuwafunza vijana wake maadili na siasa ya chama ya Ujamaa na Kujitegemea. Mkutano Mkuu wa Vijana wa Taifa uliofanyika mwaka 1983, ulisema kambi hilo liwe na kitafa na liwe linachukua vijana wa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo lilibidi litafutwe eneo ambalo ni kubwa na mahali hapo ni Ihemi.
Chuo kipo kilomita 35 kutoka Iringa Mjini kuelekea Mafinga, na wakati huo kilijulikana kama (Frontline Youth Centre Ihemi-Iringa) kilianza shughuli zake tarehe 05/11/1985 chini ya Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, kwa kushirikiana na wahisani wa shirika la msaada wa maendeleo la Denmark-DAPP (Development Aid From People to People) NGO, chini ya uongozi wa Jens Bark (mdenimark) na mkuu wa chuo wa kwanza mtanzania alikuwa marehemu hayati Omary Biabato.
Mwaka huo 1985, aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa ndugu, Mohamed Seif Khatibu na aliyekuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa ndugu hayati Joseph Lulandala, walishirikiana na kupata eneo kwa ajili ya miradi ya UVCCM, jukumu hilo walipewa na Baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere. Baada ya kupata eneo la Ihemi, Baba wa Taifa, Bwana Julius Kambarage Nyerere aliwaunganisha UVCCM na wahisani kutoka shirika la DAPP na kufanya miradi mbalimbali, lakini wahisani waliondoka mwaka 1989 na UVCCM iliizamika kuendesha chuo cha Ihemi wenyewe. Mwaka 1991 ilikuja shirika lingine la Kijerumani, 'Germany Volunteer Service' na ilikabidhiwa kuendesha chuo cha Ihemi. Mnamo Novemba 1992, shirika hilo pia liliondoka nchini, na UVCCM iliendelea kuendesha chuo cha Ihemi.
Mwaka 1986 chuo kilianza mafunzo rasmi yaliyotolewa kwa vijana wa kitanzania nchi nzima Tanzania Bara na Visiwani. Mafunzo hayo yalitolewa kwa muda wa miaka miwili na vijana waliewza kufanya mitihani ya kitaifa (Trade Test Three) katika fani zifuatazo:
1. Ufundi seremala
2. Umakanika wa magari
3. Uashi/Ujenzi
4. Ufundi umeme wa majumbani
5. Ushonaji
6. Kilimo na mifugo
Katika kuimarisha mafunzo ya ziada masomo kama vile Kiingereza, Hisabati, Uraia na Uchumi, yalifundishwa na pia wanachuo walifanya mafunzo ya (mgambo) kwa miezi mitatu. Katika kipindi hicho chuo kilikuwa kinatoa vyeti vya mafunzo kupitia VETA.
Baada ya Wafadhili kuondoka, chuo kiliendeshwa na Makao Makuu ya UVCCM Taifa na mnamo Mei, 1999 chuo kilisitisha kutoa Mafunzo kutokana na kukosa fedha za uendeshaji, fedha za mishahara ya wakufunzi na watumishi wengine. Ukosefu wa chakula kwa wanafunzi, hatimisho ikawa ni kuwasambaza wanafunzi katika vyuo tofauti ili wakamalizie mafunzo yao.
Kwa takribani miaka 15, chuo hakikuwa na shughuli rasmi za mafunzo hadi ilipofika mwaka 2016 ulipotokea msukumo kutoka katika chama wa kukifufua ili kiendelee kutoa mafunzo kwa viongozi, watendaji, wanachama na makada sambamba na kujimarisha kiuchumi kwa kutumia rasilimali ardhi iliyopo. Hivyo chama kiliunda Bodi ya Mpito ya kusimamia chuo hicho ili kisimame.
Hitimisho
Aidha, Ndugu Jokate Mwegelo alitoa pongezi kwa uongozi na wafanyakazi wa chuo hicho na akaahidi ushirikiano wa hali ya juu katika kuendeleza na kuboresha chuo hicho.
Ndugu Jokate Mwegelo alisema, "Tumekuja hapa kutathmini fursa za kuendeleza kituo chetu cha Ihemi, na hivi karibuni tutakuwa na mafunzo kwa viongozi wetu wa wilaya kutoka kote nchini."
Aidha, ningeshauri uongozi wa UVCCM kutafuta njia za kuhakikisha chuo hicho kinatoa mafunzo kwa viongozi vijana waliopo serikalini, katika sekta binafsi, na kwa wajasiriamali pia. Ninaamini kuwa mafunzo ya uzalendo, kujituma, na kujitoa ni muhimu kwa kila kijana, hasa katika nyakati hizi ambapo idadi ya vijana nchini ni kubwa zaidi.
Imeandikwa na Thomas Joel Kibwana