Makatibu Wakuu CCM
Leo tarehe 15 Januari, 2024, chama tawala cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina tarajia kumtaja Katibu Mkuu wao mpya ambae ndio atakua wa 12 tangu chama hicho kuasisiwa mwaka 1977.
Kwenye nyuzi hii nitaorodhesha watu wote waliowahi kushika nafasi hiyo kwa nyakati tofauti.
1. Pius Msekwa (1977-1981)
Pius Msekwa alikua "golden boy" wa kipindi tu baada ya Tangayika kupata uhuru.
Mwaka 1960 akiwa na umri wa miaka 25 alichaguliwa kuwa karani wa Bunge la Tangayika
Mwaka 1965 akiwa na umri wa miaka 29 alichaguliwa kuwa karani wa uchaguzi wa kwanza baada ya muunganiko wa nchi za Tanganyika na Zanzibar.
Mwaka 1967 akiwa na umri wa miaka 32 alichaguliwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa chama cha TANU.
Mwaka 1997 akachaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa CCM.
Aliendelea kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi kama vile Naibu Spika wa Bunge (1991-1994) na Spika wa Bunge (1995-2005).
2. Daudi Mwakawago (1981-1982)
Daudi alishika nafasi ya Katibu Mkuu kwa muda mfupi akionekana kama kishika nafasi wakati mrithi haswa wa Msekwa akitafutwa.
Ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na serikali.
Alikuwa Katibu wa Uenezi wa Kisiasa na Uhamasishaji wa Umma, kuanzia mwaka 1983 hadi 1987. Kuanzia mwaka 1988 hadi 1991, alikuwa Katibu wa Kamati ya Kudhibiti na Nidhamu ya Kamati Kuu ya Taifa ya chama tawala.
Pia amewahi kuwa Waziri wa Habari na Utamaduni (1982-1983), Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Nguvu Kazi (1983-1987) na Waziri wa Viwanda na Biashara (1987).
Ameshawahi pia kuwa balozi wetu nchini Italia (1992-1994) na mwakilishi wa kudumu Umoja wa Mataifa (1994-2003).
3. Rashid Kawawa (1982-1990)
Rashid Kawawa alikua mmoja wa waasisi wa Tanganyika na mshirika wa karibu wa Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere.
Mwaka 1962 aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa pili wa Tanganyika pale Nyerere alipo jiuzulu wadhifa huo ili kukijenga TANU mikoani.
Ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Waziri wa Ulinzi na Makamo wa Raisi wa Tanzania.
Mwaka 1985, Rashid Kawawa, Salim Ahmed Salim na Ali Hassan na Ali Hassan Mwinyi ndio walikuwa wagombea watatu waliokua wanawania kumrithi Nyerere kama raisi wa Tanzania. Kawawa alijitoa baadae akishauri raisi ajae asitoke kwenye kizazi cha wapigania uhuru.
4. Horace Kolimba (1990-1995)
Kipindi cha ukatibu mkuu wa Horace Kolimba ulitawaliwa na misukosuko mingi, kubwa kuliko yote ikiwa yeye kupishana na mwasisi wa chama Julius Nyerere hadi kufika hatuo kusema hadharani kuwa "chama kimepoteza dira".
Kolimba alitumia vyombo vya habari vya chama kujibu mashambulizi ya Nyerere dhidi yake haswa yale Nyerere alioandika kwenye kitabu cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania. Kwenye kitabu hicho Nyerere aliwashutumu Kolimba na John Malecela aliekua Makamo wa Raisi wa CCM-Bara kuwa viongozi dhaifu waliokua wakipanga njama za kuudhofisha Muungano.
Horice Kolimba alifariki 13 March 1997 katika mazingira ya kutatanisha mjini Dodoma akiwa ana jibu shutums dhidi yake mbele ya Kamati Kuu ya CCM.
5. Laurence Gama (1995-1997)
Laurence Gama ameshika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mkuu wa Mkoa Dodoma, Ruvuma, Tabora, na Morogoro na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (1975-1978). Pia alikua mbunge wa Songea Mjini (1995-2005)
6. Philip Mangula (1997-2007)
Philip Mangula ana historia ndefu ya utumishi ndani ya chama na serikali.
Mwaka 1966 alihuduria kozi ndefu ya masuala ya Siasa na Uongozi katika Chuo cha TANU, Kivukoni.
Mwaka 1967 alihudhuria mafunzo ya Kijeshi katika kambi ya jeshi la kujenga Taifa, Mgulani.
Mwaka huo huo 1967 alihudhuria kozi ya mafunzo maalum ya ualimu wa siasa kwenye chuo cha TANU cha Kivukoni.
Kati ya mwaka 1968-1977 alikua mwalimu wa siasa katika chuo cha TANU Kivukoni akishika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Idara ya Propaganda. Mwaka 1971,Aliteuliwa kwenda mstari wa mbele katika Jimbo la Cabo Delgado Msumbiji kushuhudia vita ya Ukombozi nchini humo.
Mwaka 1983-1986 alirudi katika chuo cha Kivukoni kama Makamu wa Mkuu wa chuo na Mkuu wa Mafunzo.
Philip Mangula anapewa sifa ya kuwa mmoja wa makatibu wakuu bora wa CCM.
7. Yusuf Makamba (2007-2011)
Yawezekana Yusuf Makamba ndie Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam (1997-2007) maarufu kuliko wote kupelekea mpaka kuitwa Jiji la Makamba. Alijizoelea umaarufu kwa aina yake ya kuwasilisha hotuba kwa kutumia matani na kunukuu mistari ya Biblia.
Amewahi pia kua Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Kigoma.
Mwaka 1978 alishiriki katika Vita vya Kagera dhidi ya Uganda akiwa Brigadi ya 202 chini ya Brigedia Imran Kombe. Baadae alihamishiwa makao makuu ya kamandi kuwa chini ya Moses Nnyauye aliekua Kamisaa wa Uhamasishaji.
Hata hivyo kipindi chake cha uongozi wa chama ulikua mgumu ukigubikwa na shutuma za rushwa na siasa za makundi.
8. Wilson Mukama (2011-2012)
Wilson Mukama anashikilia rekodi ya kushika wadhifa huo kwa muda mfupi zaidi. Wilson Mukama hakuonekana kumudu nafasi hiyo kwa vile hakuwa mwanasiasa wala hakuwa na mizizi ndani ya CCM. Alikua mtumishi wa umma ambae Mwenyekiti wa CCM wakati huo Ndugu Jakaya Kikwete alidhani angeleta utulivu ndani ya chama baada ya kuondolewa kwa Yusuf Makamba.
9. Abdulrahman Kinana (2012-2018)
Abdulrahman Kinana kama ilivyo kwa Philip Mangula, anatajwa kama mmoja wa makatibu wakuu bora kama sio Katibu Mkuu bora wa Chama Cha Mapinduzi.
Abdulrahman Kinana anakijua chama na anaijua serikali kindakindaki.
Ameshatumikia kama mwanajeshi ndani ya JWTZ, ameshawahi kuwa naibu waziri wa ulinzi na kwa sasa anahudumu kama Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara.
Abdulrahman Kinana huwa anatajwa kama "King Maker" ndani ya CCM kwa ajili ya historia yake ya kuwasaidia viongozi kadhaa kushika nafasi za juu.
Pale Mukama alipo shindwa, Abdulrahman Kinana aliitwa kuokoa jahazi. Nawiwa kusema Kinana asingekua Katibu Mkuu katika uchaguzi wa 2015 basi yawezekana kabisa CCM ingeshindwa.
10. Bashiru Ally (2018-2021)
Bashiru Ally ni design ya Mukama kwa maana ya kwamba hakua mwanasiasa wala kada wa chama na wala hakuwahi kushika nafasi yoyote ndani ya chama na serikali kabla ya kupewa ukatibu mkuu. Kabla ya uteuzi huo Bashiru Ally alikua mwanazuoni wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu Cha Dar Es Salaam.
Wengi wana amini Marehemu JPM alimtaka Bashiru kwa sababu alitaka outsider ambae angekua mwepesi kuendana naabadiliko aliokusudia kufanya ndani ya chama.
11. Daniel Chongolo (2021-2023)
Daniel Chongolo ndie Katibu Mkuu wa kwanza chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan.
Amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi wa Mawasiliano chini ya Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ikiwa chini ya Nape Nnyauye.
Mwaka 2016 aliteuliwa na Raisi Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Loliondo.
Mwaka 2018 akahamishiwa Kinondoni kwa wadhifa huo huo wa ukuu wa wilaya.
Chongolo amewahi kushika nafasi zingine kama vile Mhariri wa Radio Uhuru inayo milikiwa na CCM.
Disemba mwaka 2023, Daniel Chongolo alijiuzulu nafasi hiyo baada ya kashfa mbalimbali zilizo husishwa nae kusambaa mitandaoni.
Tangu ajiuzulu, umma haujapata kumsikia wala kumuona Daniel Chongolo.
Thomas Joel Kibwana.