Je ni Wakati wa Kumrudishia Rais wa Zanzibar Hadhi ya Umakamu wa Raisi Muungano?
Picha kutoka katika ukurusa wa Haki Ngowi
Baada ya muungano wa Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanzania ilikua na makamu wa rais wawili, wa Kwanza na wa Pili mpaka ofisi hizo zilipo unganishwa 1995. Katiba iliainisha kua endapo Rais wa Tanzania angetokea Bara basi Rais wa Zanzibar angekua Makamu wa Kwanza wa Rais na kama Rais wa Tanzania angetokea Zanzibar basi Rais wa Zanzibar angekua Makamu wa Rais wa Pili. Makamu wa Rais wa Kwanza ndio alikua na haki kikatiba kumrithi Rais wa Tanzania endapo angefariki madarakani.
Juzi kati Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mh. Hussein Mwinyi aliondoka nchini kuelekea Msumbiji kwenda kuiwakilisha Tanzania katika mkutano wa SADC unaofanyika jijini Maputo. Alipofika alipokelewa na Waziri wa Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto wa Msumbiji.
Hili jambo likanifikirisha. Nikasema cha kwanza, ni vyema sana Rais wa Zanzibar kupata fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika lengo la kudumisha Muungano ila ingependeza na kua na nguvu zaidi angeenda akiwa na cheo kinacho wawakilisha Watanzania wote. Pili, naamini kabisa Rais Mwinyi angekua na hadhi ya Makamu wa Rais wa Tanzania basi bila shaka angepokelewa uwanja wa ndege wa Maputo na mtu mwenye hadhi ya juu ya waziri au kama ni waziri basi ingekua waziri wa mambo ya nje.
Hata kwa ndani ya Tanzania, rais wa Zanzibar kikatiba ni mjumbe wa baraza la mawaziri la muungano. Ila katiba haiweki wazi rais wa Zanzibar ana hadhi gani ndani ya baraza hilo, aidha ni kama waziri au kama ni juu ya mawaziri ana nafasi gani ukilinganisha na makamu wa rais na waziri mkuu wa serikali ya muungano. Protokali hizi zote zina tatulika kwa kumpa rais wa Zanzibar hadhi ya makamu wa rais wa jamhuri. Na hili halita ongeza gharama zozote za kiutendaji na kiuendeshaji.
Kwa sasa inawezekana rais wa Zanzibar anawakilisha Tanzania kama mjumbe wa baraza la mawaziri. Ina maana akiwa nje anachukuliwa na wenyeji kwa hadhi ya uwaziri. Ila sote tunajua hadhi ya rais wa Zanzibar ni zaidi ya waziri ndio maana awapo Tanzania hupewa ulinzi na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, anapewa ADC, anaishi Ikulu, ana nguvu ya kuteua wakuu wa mikoa na wilaya, na hadhi zingine zinazo endana na za mkuu wa nchi.
Mwisho kabisa, kumpa rais wa Zanzibar hadhi ya umakamu wa rais itasaidia kudumisha muungano. Itampa uhalali wa rais wa Zanzibar kuhusika moja kwa moja na maswala ya Tanzania. ikiwa ni pamoja na kupewa heshima stahiki anapoiwakilisha Tanzania nje ya nchi.
Thomas J. Kibwana