Thomas Joel Kibwana
3 min readJan 7, 2024

--

Historia ya Sera ya Mambo ya Nje Tanzania

Diplomasia na sera ya kigeni ya Tanzania inasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje. Kuanzia uhuru mwaka 1961 hadi Desemba 1963, mambo ya nje yalikuwa idara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mwaka 1964, idara hiyo ilipandishwa hadhi na kuwa wizara kamili, ikipewa jina la Wizara ya Mambo ya Nje.

Kwa miaka arobaini tangu miaka ya sitini, shughuli za Wizara zilielekezwa na Mzunguko wa Rais Nambari 2 wa mwaka 1964 yani Presidential Circular No. 2 of 1964.

Tafsiri ya malengo makuu ya sera ya mambo ya nje chini ya Presidential Circula No.2 yalikua:

Ulinzi wa uhuru, haki na usawa: Kuhakikisha watu wanafurahia uhuru wao, wanapata haki sawa na wanaheshimiwa bila ubaguzi.

Kulinda uhuru wa taifa, mipaka na uhuru wa kisiasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Kudumisha utambulisho la taifa, mipaka yake na uwezo wa kujiendesha bila shinikizo kutoka nje.

Kuuunga mapambano dhidi ya ukoloni, ubaguzi wa rangi na ukoloni mamboleo: Kusaidia nchi na watu wanaopigania uhuru wao dhidi ya utawala wa kigeni, ubaguzi wa rangi na utawala wa kibeberu.

Kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa duniani: Kutoa misaada na kuonyesha mshikamano na watu wanaokandamizwa na kunyimwa haki zao duniani kote.

Kukuza umoja wa Afrika: Kuhamasisha na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika kwa manufaa ya pamoja.

Kukuza heshima kwa kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine: Kutoingilia shughuli za ndani za nchi nyingine bila ruhusa yao.

Kuuunga mkono sera ya kutojihusisha na upande wowote katika vita vya kimataifa: Kukaa nje ya makundi ya kijeshi yanayopigana kimataifa na kudumisha uhusiano mzuri na pande zote.

Kuuunga mkono Umoja wa Mataifa katika juhudi zake za kufikia amani na usalama wa dunia: Kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kulinda amani na utulivu duniani.
Kukuza ujirani mwema: Kudumisha uhusiano mzuri na wa kirafiki na nchi jirani.

Ni kupitia muongozo huo Tanzania ikafanya yafuatayo:

1. Tukawa miongoni mwa waasisi wa Shirika la Umoja wa Afrika, lililoanzishwa mwaka 1963.
2. Tukatumia sauti yetu, ardhi yetu na rasilimali zetu kuleta ukombozi katika nchi za Afrika ambazo bado zilikuwa chini ya ukoloni.
3. Tukapigana vita na Uganda kumuondoa Idd Amin ili kulinda mipaka yetu.
4. Tukajiunga na nchi zisizofungamana na upande wowote, yaani Harakati ya Nchi Zisizojiunga na Vikundi (Non-Aligned Movement).
5. Tukawa nchi ya kwanza ya Kiafrika kufungua mahusiano ya Kidiplomasia na mamlaka ya Palestina; japo wakati wa vita kati ya Tanzania na Uganda wakawa upande wa Idi Amin.

Kosa kubwa la kidiplomasia Tanzania iliofanya kipindi hiki ni kutetea harakati za Biafra kujitenga na Nigeria. Nchi zingine tatu tu barani Afrika ziliitambua Afrika ambazo zilikua ni Ivory Coast, Zambia na Gabon.

Nyerere alikiri kua uamuzi wa kuwa upande wa Biafra haukuwa rahisi na kwamba ilikua kosa.

Sera ya mambo ya nje tulionayo sasa imeanza kutumika mnamo mwaka 2001. Hii ilitokana na mabadiliko ya hali ya dunia ikiwemo kuisha kwa Vita Baridi, utandawazi na mfumo wa kibepari kwenye soko la dunia.

Malengo makuu ya sera yetu ya mambo ya nje ya sasa ni:
1. Kuonyesha, kukuza na kulinda maslahi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ya URT kupitia diplomasia ya uchumi yenye nguvu na endelevu
2. Kuhakikisha kuwa uhusiano wa URT na mataifa mengine na mashirika ya kimataifa nao unaendeshwa sambamba na maslahi ya kiuchumi
3.Kujenga uchumi unaojitegemea, kudumisha amani na usalama wa taifa pamoja na kuunga mkono juhudi za kikanda na kimataifa za kujenga dunia bora na yenye amani
4.Kuharakisha ushirikishwaji wa kiuchumi wa kisiasa na kijamii katika kanda
5. Kujenga mazingira yanayowezesha URT kushiriki kwa ufanisi katika uchumi wa kikanda, kimataifa na mazungumzo ya kimataifa.

Kwa muktadha huo, sera ya diplomasia ya uchumi ambayo sasa inatiliwa mkazo na serikali ya awamu ya sita chini ya Raisi Samia Suluhu Hassan sio jambo wala wazo jipya katika sera ya mambo ya nje ya Tanzania bali ni muendelezo wa sera iliokuepo lakini ikapewa kipaumbele tofauti kutokana na raisi aliepoa madarakani.

Swali ni je sera ya mambo ya nje ya sasa imefanikiwa kwa kiasi gani kutimiza malengo? Nini kiongezwe au kupunguzwa katika sera ya mambo ya nje ya sasa?

--

--

Thomas Joel Kibwana

Political enthusiast. International Relations graduate. A fan of everything Tanzania.