Heri ya Siku ya Baba Duniani
Jana ilikua siku ya baba inayo adhimishwa kimataifa Jumapili ya tatu ya mwezi wa 6 kila mwaka. Kwa bahati nzuri siko hio kwa mwaka huu iliangukia siku ya kumbukizi yangu ya kuzaliwa kwa hio sikupata muda wa kuandika jana kwa kua nilikua nasheherekea na ndugu, jamaa na marafiki.
Nia na madhumuni ya kuandika nakala hii ni kuelezea umuhimu wa baba katika familia na jamii lakini kikubwa jinsi ilivyo kipindi kigumu cha mpito kutoka uvulana kwenda kua baba. Mchekeshaji maarufu wa Marekani kwa jina la Chris Rock aliwahi kusema “only women, children, and dogs are loved unconditionally,” whereas “a man is only loved under the condition that he provide something.” Yani ni wanawake, watoto na mbwa ndio wanapendwa pasipo masharti, mwanaume anapendwa kutokana na uwezo wake wa kutoa kitu. Hivyo basi mtoto wa kiume anakua akipendwa yeye kama yeye na anajikuta ghafla kawa mtu mzima sasa kupendwa kwake kunatokana na anacho weza kukitoa. Kwa hio ubaba nao ni kazi usio kua na shukrani maana yote unayo fanya yanaonekana ni wajibu na sio mapenzi. Ndio maana kwenye lugha yetu kuna misemo kama “nani kama mama" ila hakuna anae sema nani kama baba. Mtu anapo patwa na mshtuko husema “mama yangu!" na sio baba yangu. Hivyo basi ni muhimu kuwa elimisha vijana na kuwa andaa kisaikolojia kwamba kama baba una wajibu wa kutekeleza pasipo kutegemea wala kungojea asante.
Nasema haya nikiwa ni mtu mwenye bahati sana. Umuhimu wa baba na nafasi yake nimeiona tokea nikiwa mtoto na nimekua mtu mzima nimepata mtoto na mtu ambae anashukuru na kuheshimu nafasi yangu kama baba na hili hunipa moyo na matumaini ya kuzidi kupambama. Ila pia imanifanya niwawazie mamia ya wanaume ninao kutana nao ambao hawana bahati hio. Wapo wanao simagwa, kutukanwa ma kukejeliwa kwa kidogo wanacho leta na kudhihakiwa na kutuliwa umashaka uanaume wao au ubaba wao kwa kulinganishwa na wenzao ambao wana kipato zaidi na uwezo zaidi. Kama mfanyakazi wa Heineken nimekutana mara kibao katika shughuli zangu wanaume wanaokesha baa sio kwa sababu ya ulevi bali kwa kuto kutaka kurudi nyumbani. Mtu ambae anapata sifa zaidi nje kuliko ndani lazima apaone ndani pachungu na ndio hapo utaelewa maana ya msemo wa “nabii hakubaliki kwao".
Wababa wanabeba mengi kifuani mwao katika kutafutia maisha watoto wao na familia zao. Kikubwa wanacho hitaji ni upendo na kuthaminiwa na juhudi zao kuonekana hata kama juhudi hizo bado kuzaa matunda. Naamini ni wakati sasa wa kujadili nafasi ya baba katika familia na katika jamii. Najua wapo watakao sema wababa au wanaume hawapaswi kulalamika kwani wanawake wanapitia mengi zaidi kwenye jamii. Kwa hio hii wala isichukuliwe kama ushindani kati ya mama na baba, la hasha. Wote wana umuhimu wao na ndio maana ni muhimu kuhakikisha wote wanastawi kwa manufaa ya familia zao na jamii zao.
Niliona niandike hili maana jana kupitia baadhi za kurasa za Twitter kuna baadhi walikua wamevamia sikukuu ya wababa na kuifanya ajenda ya ushindanishi kati ya wamama na wababa. Wakati kinyume na hapo wanaume wangevamia sikukuu ya kina mama na wakaifanya kuhusu wao tunajua hali ingekua tofauti.
Mwisho nitoa shukrani kwa wanawake na wanamama wote wanao tambua na kuthamini mchango wa baba. Familia inajengwa na baba na mama imara na ni muhimu wote kutiwa moyo katika kutekeleza majukumu yao. Wapo mababa ambao ni single fathers na wanalea watoto wenyewe, wapo sana. Ifike wakati tutambua kua wote tuna hitaji kuinuliwa na si dhambi siku ya kinababa ikabaki ya kina baba wakati huo huo tukiendelea kupigania usawa na haki kwa jinsia zote.
Haya ni maoni yangu tu na nitafurahi kusikia maoni zaidi na kujifunza zaidi toka kwa watu wengine wenye uzoefu tofauti.
Thomas J. Kibwana.