Thomas Joel Kibwana
4 min readNov 5, 2022

Dr. Hussein Mwinyi na Miaka Miwili ya Uongozi Wake.

Leo inatimia miaka miwili tangu kuanza rasmi uongozi wa Dr. Hussein Mwinyi kama Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Ni miaka miwili ambayo imemulika mwanga si kwa Wazanzibari tu bali kwa Watanzania kiujumla kwa aina ya uongozi (leadership style) ya Raisi Mwinyi. Niwe mkweli, mwaka 2020 wakati wa mchakato wa uraisi wa Zanzibar CCM nilitamani Mwinyi ashinde na tangu aanze uongozi wako amedhihirisha kwa nini alikua mtu sahihi kwa nafasi hiyo.

Naomba niainishe machache tu niliyo yaona kwa Raisi Mwinyi ambayo yana dhihirisha umahiri wake katika uongozi. Haya ni maoni binafsi na wengine wapo huru kutoa tafsiri yao au hukumu yao juu ya uongozi wake.

1. Upatanishi na usuluhishi:
Uchaguzi wa uraisi Zanzibar mwaka 2020 ulikua wamoto sana. Mbambano kati ya Dr. Hussein Mwinyi na Maalim Seif Sharif Hamad uliinua shauku ya hata Watanzania wa upande wa pili wa Muungano. Ni uchaguzi ambao Bwana Hamad aliapa hato kubali kushindwa na hato kubali serikali ya umoja wa kitaifa (SUK). Kauli hio ilifanya uchaguzi upande wa Zanzibar uwe wa moto sana huku watu wakihofia nini kingetokea baada ya uchaguzi.

Tarehe 28 Oktoba wa mwaka 2020 uchaguzi ukafanyika Zanzibar na Dr. Hussein Mwinyi akatangazwa kama mshindi kwa asilimia 76 za kura. Yaliofuata ni mazungumzo kati ya Dr Hussein Mwinyi/CCM na Seif Sharif Hamad/ACT yalioisha kwa kuundwa kwa SUK na Bwana Hamad kuapishwa kama Makamo wa Kwanza wa Raisi Zanzibar. Kumbuka ilikua miaka mitano tu nyuma ambapo Seif Sharif Hamad aligomea kushiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar na kukataa kua sehemu ya SUK.

Hapa nipongeze busara na hekima za wote Raisi Mwinyi na Hayati Seif Sharif Hamad. Ila tukio hili lili dhihirisha imani Seif Sharif Hamad aliokua nayo juu ya Raisi Mwinyi na imani yake kwamba huyu ni mtu ambae angeweza fanya nae kazi. Na tangu wakati huo Raisi Mwinyi amehakikisha joto la siasa za uchaguzi Zanzibar umeisha na Wazanzibari wanasonga mbele kwa pamoja.

2. Mahusiano ya Kimataifa:
Tangu nimepata akili nimeshuhudia maraisi wanne wa Zanzibar ambao ni Salmin Amour, Amani Abeid Karume, Dr. Mohamed Ali Shein na sasa Dr. Hussein Mwinyi. Katika maraisi hao wote, ukizingatia mfumo wa Muungano wenye raisi wa Jamhuri ya Muungano na Makamo wa Raisi na waziri wa mambo ya nje, ni mara ya kwanza kuona raisi wa Zanzibar akiiwakilisha serikali ya Jamhuri ya Muungano kwenye shughuli mbali mbali za kimataifa.

Japo Raisi wa Zanzibar kwa nafasi yake anakua mjumbe wa Baraza la Mawaziri ila ni nadra sana kusikia Raisi wa Zanzibar anaenda nje kuiwakilisha Tanzania katika mikutano mbali mbali ya kikanda na kimataifa. Hakika sikuliona hili kwa watangulizi wake. Hili lina dhihirisha imani ambayo serikali ya Jamhuri ya Muungano inao juu ya uwezo wake na hakika umuhimu wake katika kuiwakilisha nchi kiujumla.

3. Maono ya kiuchumi:
Tangu kuingia kwa Raisi Mwinyi madarakani unaona kabisa nia ya dhati ya kuleta mapinduzi katika uchumi wa Zanzibar. Leo hii tunaona kidogo kidogo Zanzibar ikianza kushindana na Nairobi kama kitivo cha kampuni za tehama. Tumeshuhudia Wasoko ikihamisha makao makuu yake na uongozi wake wa juu toka Nairobi kwenda Zanzibar. Tunaona serikali ya Zanzibar inavyo tafuta misaada ya kimkakati toka nchi rafiki na Zanzibar. Tunaona maboresha katika mazingira ya uwekezaji Zanzibar. Tumeona maboresho kwenye airport ya kimataifa ya Abeid Amani Karume na uwekezaji wa nje unaofanyika ambao kwa hakika itapelekea Zanzibar kufunguka zaidi kimataifa.

Yote hapo juu bado hatuja zungumzia mkakati wa uchumi wa bluu ambao ni mkakati unaolenga kuinufaisha Zanzibar na moja ya rasilimali zake kuu ambayo ni maji ya bahari. Majini kuna mafuta ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Muungano imekubaliana kua hilo liwe jambo la Zanzibar na si la nchi kitu ambacho Wazanzibari wengi walikua wanalilia. Majini kuna samaki wanaoweza vuliwa kama chanzo cha biashara Zanzibar. Na majini kunatoa fursa ya uwekezaji kwenye utalii Zanzibar.

Nina amini na mikakati hii ya kiuchumi yakiweza kutekelezeka hata kwa asilimia 50 basi Zanzibar miaka 10 ijayo itakua sehemu tofauti kabisa na sasa kiuchumi. Yote haya yakiwa chini ya maono ya Raisi Hussein Mwinyi.

Hayo ni machache tu ambayo nimeyaona kwa Raisi Mwinyi yanayo nipa imani kwamba uongozi wake si tu utainufaisha Zanzibar bali utainufaisha Zanzibar kiujumla. Natamani kwa sasa tuone kwenye kila ubalozi wa Tanzania afisa wa Zanzibari ambae atakua anashughulikia tu maswala ya Zanzibar haswa kwenye kuitangaza Zanzibar na kuitafutia Zanzibar fursa za kiuchumi.

Nina imani kwamba Raisi Mwinyi ana nia ya dhati na Zanzibar na nia ya dhati ya kuifungua Zanzibar kiuchumi na kijamii. Unapo angalia uongozi wa Raisi Mwinyi unaona mtu aliekaa na kutafakari mipango sahihi kwa ajili ya Zanzibar kabla haja amua kugombea uongozi wa juu wa Zanzibar. Na nina imani kabisa ataiacha Zanzibar katika hali bora zaidi kuliko alivyo ikuta. Akiwa ana adhimisha miaka miwili ya uongozi wake namtakia afya njema na busara katika utekelezaji wa majukumu yake kwa miaka aliyo bakisha.

Thomas Joel Kibwana

Thomas Joel Kibwana

Political enthusiast. International Relations graduate. A fan of everything Tanzania.